Siku ya Mazingira Duniani Mwaka wa 2023 

KAULIMBIU: ##KOMESHAUCHAFUZIWAPLASTIKI 

Kaulimbiu ya Siku ya Mazingira Duniani Juni 5, mwaka wa 2023 iliangazia masuluhisho ya uchafuzi wa plastiki chini ya kampeni ya #KomeshaUchafuziWaPlastiki. Dunia inasakamwa na plastiki. Ni bei nafuu kuitengeneza, hudumu, ni rahisi kubadilishwa, na rahisi kuisafirisha. Lakini kiasi kikubwa cha plastiki zinazotengenezwa na kutupwa kila mwaka kina athari mbaya kwa mifumo  yetu ya ekolojia, kwa wanyamapori, kwa afya ya binadamu na kwa uchumi. 

Mabadiliko ya mifumo yanahitajika ili kushughulikia chanzo cha uchafuzi wa plastiki. Hii itaanza na kupunguza matumizi ya plastiki inayosababisha matatizo na isiyohitajika, kuitumia tena na kujaza bidhaa zilizopo ili kuepukana na utamaduni wa kutupa, na kubadilisha mifumo, bidhaa na mifuko ya kufungia.    

ATHARI ZA JANGA LA UCHAFUZI WA PLASTIKI 

Takribani tani milioni 430 za plastiki hutengenezwa kila mwaka, nusu yake ikiwa imeundwa kutumika mara moja tu. Kati ya hiyo, chini ya asilimia 10 huchakatwa. Kila mwaka takribani, tani milioni 4 za taka za plastiki husafirishwa nje ya nchi kutoka nchi zenye kipato cha juu hadi nchi zenye kipato cha chini na cha kati, zilizo na miundomsingi chache ya kushughulikia taka kwa njia inayojali mazingira. Kati ya plastiki zinazotengenezwa duniani, wastani wa kati ya  tani milioni 19 na 23 hujikuta kwenye maziwa, mitoni na baharini. Sasa, plastiki huziba madampo yetu, huingia baharini na kuchomwa na kutoa moshi wenye sumu, na kuifanya kuwa mojawapo ya vitishio vikuu kwa sayari. Sio hayo tu, kile ambacho hakijulikani ni kwamba maikroplastiki hujikuta katika chakula tunachokula, hewa tunayovuta, maji tunayokunywa na hata kwa hewa tunayopumua. Bidhaa nyingi za plastiki huongezwa vitu hatari, ambavyo vinaweza kuwa tishio kwa afya yetu ikiwa ni pamoja na kuongeza uwezekano wa kupata magonjwa ya moyo na kuzidisha matatizo ya kupumua.   

MASULUHISHO 

Habari njema ni kwamba tuna sayansi na masuluhisho ya kushughulikia janga hili - na mengi tayari yanafanyika. Kwa mfano, kutumia mbinu ya mzunguko mzima ni muhimu ili kuweza kukomesha uchafuzi wa plastiki na kupunguza gharama kwa mazingira, kwa jamii, na kwa uchumi. Kama sehemu ya mbinu ya mzunguko mzima, juhudi hazielekezwi tu kwa kudhibiti taka, bali kwa kuchunguza jinsi bidhaa zinavyoundwa, kutengenezwa na kusambazwa. Kubadilisha jinsi tunavyozalisha, kutumia, kurejesha na kutupa plastiki kunaweza kuokoa Dola za Marekani trilioni 4.5 trilioni kufikia mwaka wa 2040. Na ingawa watu wengi wanafikiri kuhamia nishati jadidifu na vitu mbadala vinayoweza kuoza ni chaguo endelevu, chaguo bora zaidi ni kutumia plastiki chache, bila kujali nyenzo zilizotumika kutengeneza vitu vinavyoweza kutumika tena.   

UMUHIMU WA KUCHUKUA HATUA ZA DHARURA 

Kinachohitajika zaidi sasa ni kuongezeka kwa shinikizo kutoka kwa umma na wanasiasa kuimarisha na kuharakisha hatua kutoka kwa serikali, kampuni na washikadau wengine ili kutatua janga hili. Hii inaonyesha umuhimu wa Siku ya Mazingira Duniani kuhamasisha hatua kuchukuliwa kutoka pembe zote duniani. Siku ya Mazingira Duniani mwaka wa 2023 ilionyesha jinsi nchi, mashirika ya biashara na watu binafsi wanavyojifunza kutumia nyenzo kwa njia endelevu zaidi, na kutoa matumaini kwamba siku moja, uchafuzi wa plastiki utazikwa katika shimo la sahau. Siku hiyo pia ilikuwa maarufu sana miongoni mwa umma, na kuvuma kama hashtagi #1 na #2 kwa Twitter tarehe 5 Juni.  Pia kulikuwa na matamanio duniani ya kujifunza zaidi kuhusu masuluhisho ya washikadau ya kukabiliana na uchafuzi wa plastiki yaliopelekea kupakuliwa mara 63,000 kwa Mwongozo wa Vitendo wa Kukomesha Uchafuzi Wa Plastiki na kutajwa zaidi ya mara 53,000 katika machapisho mapya katika nchi 167.    

NCHI MWENYEJI 

Siku ya Mazingira Duniani Mwaka wa 2023 iliandaliwa na Côte d'Ivoire kwa ushirikiano na Uholanzi. 

Huwa mstari mbele kwa kampeni dhidi ya uchafuzi wa plastiki. Tangu mwaka wa 2014, Côte d'Ivoire ilipiga marufuku matumizi ya mifuko ya plastiki, na kuwezesha mabadiliko ya kutumia mifuko ya plastiki inayoweza kutumika tena. Jiji kubwa zaidi nchini humo, Abidjan, pia limekuwa kitovu cha waanzilishi wa kampuni wanaojali mazingira. Serikali ya Uholanzi pia iliunga mkono Siku ya Mazingira Duniani kama mojawapo ya nchi zinazochukua hatua kabambe za kuzingatia mzunguko mzima wa plastiki, kwa kuwa mmojawapo wa waliotia saini Ahadi Mpya ya Kimataifa ya Uchumi wa Plastiki na kuwa mwanachama wa Ushirikiano wa Kimataifa kuhusu Uchafuzi wa Plastiki na Uchafuzi wa Baharini

LINKI MUHIMU