Ujumbe mkuu
Canva

Kote ulimwenguni, mifumo ya ekolojia iko hatarini. Kuanzia kwa misitu na nchi kavu hadi kwa mashamba na maziwa, maeneo ya kiasili yanayotegemewa na binadamu kuwepo yamefikia mwisho mwa uwezo wake. Hii ndiyo sababu Siku ya Mazingira Duniani  inaangazia uboreshaji wa ardhi, kukomesha kuenea kwa majangwa  na kujkuza ustahimilivu dhidi ya ukame chini ya kaulimbiu “ “Ardhi Yetu. Mustakabali wetu. Sisi ni #GenerationRestoration.””  

 Uboreshaji bora wa ardhi unahitaji mbinu inayotumia maarifa, msukumo na kujitolea kwa vizazi vyote. Kila mtu aliye hai kwa sasa ni sehemu ya kizazi ambacho ni cha kwanza kushuhudia athari mbaya zaidi za uharibifu wa mazingira na cha mwisho kuchukua hatua za kukabiliana nazo ili kuwezesha kufikia malengo ya kimataifa kuhusu tabianchi na bayoanuai. Tunaweza kuwa kizazi ambacho hatimaye kitafanya amani na ardhi. Tunaweza kuwa #GenerationRestoration.   

Ukame, kuenea kwa majangwa na uharibifu wa ardhi ni tishio linaloongezeka kwa sayari na watu.  

  • Kote duniani, zaidi ya hekta bilioni 2 za ardhi zimeharibiwa - eneo linalokaribia ukubwa wa India na Shirikisho la Urusi kwa pamoja. 
  • Kila mwaka, inakadiriwa kuwa hekta milioni 12 za ardhi  hupotezwa kupitia uharibifu, na kuathiri usambazaji wa chakula na maji kote ulimwenguni.  
  • Watu milioni 55 huathiriwa moja kwa moja na ukame kila mwaka, na kuufanya kuwa tishio kubwa zaidi kwa mifugo na mazao karibu kila sehemu ya dunia.  

Kutoweka kwa ardhi iliyokuwa ikitumika huathiri vibaya wale wasiokuwa katika hali nzuri. 

  • Uharibifu wa mifumo ya ekolojia huathiri watu bilioni 3.2, au asilimia 40 ya jumla ya idadi ya watu wote duniani.  Hudhuru vibaya wale ambao hawana uwezo mkubwa wa kustahimili: jamii za vijijini, wakulima wadogowadogo na maskini.  
  • Uharibifu wa ardhi unaweza kupunguza uzalishaji wa chakula kwa asilimia 12 duniani, na kusababisha bei ya vyakula kupanda hadi kwa asilimia 30 kufikia mwaka wa 2040.  
  • Kufikia mwaka wa 2030, ukame, uharibifu wa ardhi na kuenea kwa majangwa kunaweza kulazimisha watu milioni 135 kuhama huku janga la mabadiliko ya tabianchi likizidi kuwa baya zaidi. Uharibifu wa ardhi ni tishio kwa haki za kuishi, kuwa na afya, kuwa na chakula, kuwa na maji na kuwa na mazingira mazuri.   
  • Vijana ni sehemu ya kundi linalokua la waliohama bila hiari wanaojulikana kama ‘watu waliohamishwa na mazingira’ kwa sababu uharibifu wa mazingira unaochochewa na mabadiliko ya tabianchi huwalazimu kuhama kutokana na kutokuwa na uwezo wa kujikimu kupitia ardhi yao. 
  • Katika mazingira tete, uharibifu wa ardhi unaweza kuchochea mizozo na vurugu kutokana na kupoteza makao na ushindani wa rasilimali chache kati ya makundi mbalimbali katika jamii kama vile wakulima na wafugaji.    

uchumi duniani unaumia kutokana na shinikizo la ukame na uharibifu wa ardhi. 

  • Inakadiriwa kuwa dola trilioni 10 za Marekani za jumla ya Pato la Taifa zinaweza kupotea kufikia mwaka wa 2050 ikiwa huduma za mifumo ya ekolojia zitaendelea kudidimia.  
  • Kote duniani, hekta milioni 12 za ardhi  zilizo na uwezo wa kuzalisha tani milioni 20 za nafaka hupotea kutokana na ukame na kuenea kwa majangwa kila mwaka, na hivyo kusababisha uhaba wa chakula kwa mamilioni ya watu.  
  • Uharibifu wa ardhi unaweza kuathiri michakato asilia Duniani, na kusababisha  mmomonyoko wa udongo na uhaba wa maji safi.  Pia ndicho chanzo cha janga linalopelekea spishi milioni 1 kutoweka.  

Mabadiliko ya tabianchi na mfumo mbofu wa chakula huzidisha mali ya ukame na kuenea kwa majangwa.  

  • Mabadiliko ya tabianchi huzidisha makali ya kuenea kwa majangwa na uharibifu wa ardhi kwa kuongeza umaratokezi na makali ya ukame, mawimbi ya joto na mioto misituni.    
  • Ukataji miti na uharibifu wa udongo huzidisha mabadiliko ya tabianchi kwa kuharibu misitu, maeneo yaliofunikwa na nyasi ambayo ni hifadhi kuu za molekuli za hewa ya ukaa zinazoongeza joto katika sayari.   
  • Kilimo ndicho kichocheo kikuu cha uharibifu wa ardhi. Upanuzi wa kilimo umeondoa au kubadilisha takribani asilimia 70 ya maeneo yaliofunikwa na nyasi na asilimia 50  ya savana kote duniani. 

Ili kukabiliana na kuenea kwa majangwa na uharibifu wa ardhi, ulimwengu ni sharti uboreshe mifumo ya ekolojia iliyoharibiwa. 

  • Kila dola inayowekezwa katika uboreshaji wa mifumo ya ekolojia—mchakato wa kusitisha na kukabiliana na uharibifu—hupelekea hadi dola za Marekani 30 kupitia huduma za mifumo ya ekolojia, na husaidia ulimwengu kufikia  Malengo ya Maendeleo Endelevu, mwongozo wa wanadamu wa kuwa na mustakabali bora. 
  • Kurejesha asilimia 15ya ardhi ambayo matumizi yake yamebadilishwa kataka maeneo mwafaka kunaweza kuzuia asilimia 60 ya kutoweka kwa viumbe wanaotarajiwa kuangamia.  
  • Uhifadhi na uboreshaji wa mifumo ya ekolojia  kunaweza kusaidia kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na majanga yanayohusiana tabianchi kwa kuhuisha uwezo kamili wa misitu, maeneo ya mboji, maeneo yaliokauka, ardhioevu na mito, kuhifadhi hewa ya ukaa, kupunguza uzalishaji wa gesi ya ukaa na kustahimili athari za majanga. 
  • Miji hukalia asilimia tatu tu ya ardhi Duniani, lakini ni makazi kwa zaidi ya nusu ya watu duniani. Ni nguzo kuu kwa mifumo ya ekolojia duniani na kuchangia takribani asilimia 75 ya matumizi ya rasilimali na nishati duniani; huzalisha zaidi ya nusu ya taka duniani; na angalau asilimia 60 ya uzalishaji wa gesi ya ukaa. Kutokana na athari yake kubwa, miji inaweza kutekeleza wajibu muhimu katika juhudi za kuboresha na kukuza uwezo wa kustahimili ukame.    

Kote duniani, kumekuwa na maendeleo ya kutia moyo katika miaka ya hivi karibuni katika juhudi za kuboresha mandhari yaliyoharibiwa. 

  • Nchi zinapiga hatua katika utekelezaji wa ahadi zake chini ya Muongo wa Umoja wa Mataifa wa Kuboresha Mifumo ya Ekolojia, juhudi za kimataifa za kuhuisha maeneo ya kiasili. Nchi zimeapa kuboresha hekta bilioni 1 za ardhi iliyoharibiwa na kutoa ahadi sawia kwa maeneo ya baharini na pwani. 
  • Kwa sasa, kati ya hekta milioni 765 na bilioni 1 zimetengwa kwa ajili ya uboreshaji. Takriban nusu ya eneo litakaloboreshwa lipo Kusini mwa Jangwa la Sahara, kukiwa na kujitolea pakubwa pia katika maeneo ya Asia na Amerika ya Kusini.  
  • Muongo wa Umoja wa Mataifa wa Kuboresha Mifumo ya Ekolojia Miradi Mikuu ya Uboreshaji wa Mifumo ya Ekolojia Duniani—msururu wa mipango anzilishi—tayari unaonyesha jinsi uboreshaji unavyozalisha manufaa mbalimbali kwa mazingira, ikiwa ni pamoja na kuongezeka kwa mazao, ufyonzaji wa hewa ya ukaa na uhifadhi wa bayoanuai.  
  • Mfumo wa Kimataifa wa Bayoanuai wa Kunming-Montreal, mkataba wa kihistoria wa kutunza mazingira uliotiwa saini mwaka wa 2022, unajumuisha shabaha kuwa kufikia mwaka wa 2030 angalau asilimia 30 ya nchi kavu iliyoharibiwa, na mifumo ya ekolojia ya maeneo ya bahari na pwani yanaendelea kuboreshwa ipasavyo. 

Siku ya Mazingira Duniani ni fursa ya kuangazia masuluhisho ya ukame, kuenea kwa majangwa na uharibifu wa ardhi. 

  • Tangu mwaka wa 1973, Siku ya Mazingira Duniani (WED) , imehamasisha kuhusu masuala muhimu ya mazingira, kuanzia na mabadiliko ya tabianchi hadi kwa kupungua kwa tabaka la ozoni. Siku hii imesaidia kuchochea serikali, mashirika ya biashara, makundi ya mashirika ya uraia na watu binafsi kuchukua hatua, na kushughulikia changamoto hizi. 
  • WED 2024 inaandaliwa na Ufalme wa Saudi Arabia itaangazia uboreshaji wa ardhi, kukomesha kuenea kwa majangwa na kukuza uwezo wa kustahimili ukame. 
  • Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP) husimamia WED, inayoadhimishwa kila mwaka tarehe 5 Juni.  

Watu wa Kiasili, wanawake na vijana hutekeleza wajibu muhimu wa kuboresha mifumo ya ekolojia ilioharibiwa na kukabiliana na uharibifu wa ardhi, kuenea kwa majangwa na ukame. 

Kila mtu anaweza kuwa sehemu ya kampeni ya WED 2024 na kuchangia katika juhudi za kuboresha ardhi kwa manufaa ya vizazi viliopo na vijavyo. 

  • Uzuri wa uboreshaji wa mifumo ya ekolojia ni kwamba unatoa ujumbe wa hatua na matumaini, na unaweza kutokea kwa kiwango chochote. Hapa kuna jinsi ya kujiunga na hatua:  
  • Jisajili na ushiriki katika shughuli, hafla au hatua za uboreshaji wa mifumo ya ekolojia kati ya Aprili na Juni. 
  • Angazia shughuli yako kwenye Ramani ya Shughuli za Siku ya Mazingira Duniani kisha upokee kadi ya usajili. 
  • Shiriki katika kazi ya uboreshaji wa ardhi na udongo kwa kutumia mwongozo wa vitendo wa UNEP.  
  • Eneza habari na kuwatia moyo wengine kwa kushiriki jinsi unavyosaidia kuhuisha ardhi, ukitumia hashtagi za #GenerationRestoration na #SikuYaMazingiraDuniani.   
  • Tembelea  tovuti ili kupata nyenzo, taarifa za hivi karibuni, matukio, habari na vidokezo. 
  • Tumia nyenzo za mawasiliano kutoka kwa kampeni na ushiriki nyenzo hizo na marafiki zako, wenzako, washirika wako na mitandao yako ili kuangazia masuluhisho na mbinu bora.  
  • Shiriki na uangazie ujumbe wa Siku ya Mazingira Duniani ndani ya jamii yako kuhusu jinsi ya kushiriki katika juhudi za kuboresha ardhi katika mazingira mbalimbali, kuanzia kwa majengo ya ofisi, shule, na bustani hadi kwa mashamba ya kilimo, mbuga, na hata barabara kuu.    
  • Alika wengine katika mitandao yako kujiandikisha na kujiunga.