Afya ya binadamu hutegemea mifumo ya ekolojia ambayo sisi sote hutegemea. Kuboresha mifumo ya ekolojia iliyoharibika - kwa mfano kwa kupanda miti, kusafisha kingo za mito, au kutoa nafasi kwa mazingira kujiboresha - huongezamanufaa yake kwa jamii na kwa bayoanuai. Bila kuboresha mifumo ya ekolojia, hatuwezi kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu au Mkataba wa Hali ya Hewa wa Paris. Lakini mifumo ya ekolojia pia ni changamano na anuwai, na uboreshaji wake unahitaji upangaji makini na uvumilivu wakati wa utekelezaji.
Ili kuhimiza uboreshaji wa mifumo ya ekolojia kila mahali, UNEP imechapisha mwongozo wa vitendo wa uboreshaji wa mifumo ya ekolojia. Uliotolewa mwanzoni mwa Muongo wa UN wa Kuboresha Mifumo ya Ekolojia, 2021-2030, Kitabu cha Mikakati ya Uboreshaji wa Mifumo ya Ekolojia kinaangazia kwa ufupi juhudi mbalimbali zinazoweza kupunguza na kukomesha uharibifu wa mifumo ya ekolojia na kuiboresha.
Ulioundwa kwa watu wote wanaopenda kushiriki na vikundi vya wadau, mwongozo unaelezea njia tatu za kushiriki Uboreshaji wa Mifumo ya Ekolojia wakati wa Muongo wa UN na baadaye:
- Kuchukua hatua kama vile kuanzisha au kujiunga mradi ulipo wa uboreshaji
- Kufanya uamuzi mzuri kama kununua tu bidhaa endelevu na kubadilisha mlo
- Kuhamasisha kuhusu uhifadhi na uboreshaji wa mifumo ya ekolojia
Mwongozo ulio na kurasa 21 unaelezea njia za kuboresha aina nane za mifumo ya ekolojia - misitu, mashamba, nyika na savana, mito na maziwa, bahari na pwani, miji na majiji, maeneo ya mboji, na milima. Pia inaelezea jinsi sehemu zote za jamii - kutoka kwa watu binafsi na vikundi vya jamii hadi wafanyabiashara na serikali - zinaweza kujiunga na #GenerationRestoration, vuguvugu la kimataifa la kuboresha mifumo ya ekolojia kila mahali kwamanufaa ya watu na mazingira.