Ajenda ya Maendeleo Endelevu ya Mwaka wa 2030 ni jukwaa la kuwezesha kila mtu kuwa salama na tajiri duniani. Lina malengo 17 yanayojulikana kama Malengo ya Maendeleo Endelevu, yanayoshughulikia changamoto za kimataifa kuhusiana na umaskini, ubaguzi, mabadiliko ya tabianchi, uharibifu wa mazingira, amani na haki. Malengo hayo huingiliana na kutegemaana: kukuza lengo mojawapo ni kukuza malengo mengine; na bayoanuai ni muhimu mno kwa malengo yote.
Bayoanuai ni muhimu kwa maendeleo na maisha ya binadamu
Bayoanuai ni nguzo ya ukuzaji wa uchumi. Zaidi ya nusu ya GDP duniani–inayokadiria takribani dola za Marekani trilioni 44–hutegemea mazingira kwa kiwango fulani au huyategemea kabisa. Kwa wale wanaoishi katika umaskini, zaidi ya asilimia 70 hutegemea kwa kiwango fulani, mali ghafi ili kupata mapato, iwe ni kupitia kwa ukulima, uvuvi, upandaji wa miti na shughuli nyinginezo zinazotegemea mazingira.
Mazingira hutoa aina nyingi ya madawa yanayotumiwa kwa tiba ya kisasa. Mimea, wanyama na vijidudu husaidia watafiti katika nyanja ya afya kuelewa fiziolojia ya binadamu na kutibu magonjwa. Watu bilioni nne hutegemea madawa ya kiasili tu, na takribaniasilimia 70 ya madawa ya saratani ni ya kiasili au sanisi kutokana na mazingira.
Mifumo ya ekolojia huboresha hali ya hewa kwa kukusanya na kuhifadhi gesi ya ukaa. Hakika, mifumo mizuri ya ekolojia inaweza kukabiliana kwa asilimia 37 na ongezeko la joto duniani. Kwa upande mwingine, tunapoharibu mifumo ya ekolojia–ikiwa ni pamoja na kwa maeneo yenye unyevunyevu, mikoko na misitu ya maeneo ya tropiki–itazalisha kaboni badala la kuihifadhi.
Mifumo anuai ya ekolojia inaweza kusaidia kupunguza athari za majanga ya kiasili kama vile mafuriko, tsunami, maporomoko ya theluji, maporomoko ya ardhi na kiangazi. Pia, yanaweza kuzuia magonjwa kuenea: maeneo ambayo yana bayoanuai ya kiasili ya kiwango cha juu, kiwango cha ueneaji wa magonjwa yanayotokana na wanyama, kama vile virusi vya COVID-19, huwa chini.
Kuyafikia malengo ya maendeleo endelevu
Madhara yanayotokana na shughuli za binadamu–mabadiliko katika matumizi ya ardhi, matumizi mabaya ya ardhi, uzalishaji wa gesi ya ukaa inayosababisha mabadiliko ya tabianchi, uchafuzi na ueneaji wa aina ya miti isiyokuwa ya kiasili–ni masuala yaliyo wazi.
Kila mwaka hekta milioni 13 ya maeneo ya misitu; na majangwa yametokea kwa hekta bilioni 3.6 ya ardhi. Asilimia 8 ya aina yote ya wanyama wameangamia na asilimia 22 ya wanyama wote wanaotambulika wamo hatarini kuangamia. Kwa sasa, uchafuzi umeharibu maji katika maeneo ya pwani; na aina nyingi ya samaki wanaangamia. Shughuli za binadamu pia zimechangiahali ambayo hupelekea virusi kusambaa kwa haraka kati ya wanyama na binadamu, na kupelekea kuzuka kwa magonjwa ambukizi kama vile COVID-19.
Kwa mjibu wa ripoti iliyochapishwa mwaka jana, hali isiyoweza kubadilishwa ya uharibifu wa mazingira ya kiasili imekuwa tishio kubwa kwa miongo miwili iliyopitalinaloathiri hatua za kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu. Licha ya hayo, bado kuna uwezekano wa kuwa na hatima nzuri, ila tunahitaji kufanyia sera ya maendeleo mabadiliko makubwa na kuchukua hatua mwafaka.
Ni wakati wa Mazingira
Tukisalia na miaka 10 ili kufikia Ajenda ya Maendeleo Endelevu, na tunapoingia Muongo wa Kuchukua Hatua za Kufikia Malengo ya Kimataifa, mwaka wa 2020 ni kigezo cha iwapo tutafaulu au tutashindwa. UNEP na wabia wake wataendeleza Muongo wa Kuboresha Mifumo ya Ekolojia; na mikutano muhimu ya kimataifa, kama vile Kongamano la Nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Bayoanuai ya Kibayolojia, utaweka mwelekeo wa hatua za kimataifa zinazopaswa kuchukuliwa.
Kukubiliana na uharibifu wa bayoanuai ni njia ya kipekee ya kuboresha na kuimarisha sayari na viumbe wote wanaopatikana ndani yake. Ni wakati wa kubadili mienendo yetu kwa mazingira na kuyafanya nguzo ya uamuzi wetu.